Home News Kilimo Ni Ajira Kubwa Kwa Vijana

Kilimo Ni Ajira Kubwa Kwa Vijana

Kama tunavyojua nchini Tanzania zaidi ya asilimia 80 ya uchumi wa nchi hutegemea na shughuli za kilimo. Vivyo hivyo akielezea Mh. Dr. Bilal kwamba asilimia 60 ya ardhi yetu ni nzuri kwenye shughuli za kilimo na haijatumika ipasavyo.  Kwa asilimia kubwa ya vijana wahitimu wa vyuo vikuu, wapo mtaani kwa kukosa ajira.

Kwa kuona tatizo hili limekithiri, Balton Tanzania ltd kama shirika binafsi limekuwa likitoa semina mbali mbali kwa makundi ya vijana kuhusiana na kilimo biashara ili kumpatia ajira mbadala kijana.

Kundi kubwa la vijana bado linaona kilimo ni utumwa na sio kama ajira zingine. Akifafanua Afisa mahusiano na biashara Bi Linda byaba, alisema “ bado kundi kubwa la jamii limekuwa likiendelea  na kilimo cha mazoe hali inayofanya wengi wao kushindwa kupata mafanikio ya haraka kama inavyokuwa ndoto yao hivyo kufanya vijana kukacha kilimo na kubaki mtaani ”

Pengine wengi bado wako gizani kuhusu ufahamu wa uwepo wa kampuni ya Balton Tanzania ambayo inajishughulisha na utoaji huduma za kilimo ikiwemo pembejeo, utaalamu wa ulimaji ili  kupata mazao bora na yenye tija sanjari na zana za kilimo.

Ni kampuni ya Israeli ambayo inafanya shughuli zake nchini kwa takribani miaka 50 sasa na imepata mafanikio makubwa makubwa kupitia  kilimo hali ambayo imekuwa ikiunga mkono juhudi za Serikali kupitia kauli mbiu ya maonesho ya nanenane 2014 “MATOKEO MAKUBWA KILIMO SASA BIASHARA.”

Balton Tanzania kwa huduma zake kwa jamii na usambazaji wa teknolojia za kilimo na za kisasa, iliibuka mshindi katika kanda ya kati, kusini na kaskazini kwenye maonesho ya kitaifa ya nanenane.

Kwa Tanzania, Balton ina ofisi zake katika Jiji la Dar es Salaam, Iringa na Arusha na tayari imeajiri watanzania wanaozidi 100 sanjari na wafanyakazi wegine wasiokuwa na ajira za kudumu.

Kwa hakika kijana ambaye anahitaji kujihusisha na kilimo pengine anaweza kuwa na maswali mengi kuhusu msaada unaotolewa Balton ili kuhakisha anapata mafanikio kupitia nyanja hiyo. Ni kwamba kampuni inatoa mafunzo na semina kuhusu hatua  zinazoweza kuchukuliwa na wakulima ili kuhakikisha wanapata mazao bora kupitia kilimo cha kisasa kwa njia ya matone.

Kutokana na kuwepo kwa semina hiyo, makundi mengi ya wakulima yamekuwa yakijitokeza katika ofisi hizo ili kuhakikisha wanapata utaalamu wa kutosha kwa lengo la kuondokana na kilimo kisichokuwa na tija.

Kwa ushuhuda wa baadhi ya wahusika wa semina hizo wapo  baadhi yao wamefanikiwa kupiga hatua kubwa katika nyanja hiyo na kuwa sehemu ya mfano kwa wengine wenye mahitaji ya kuingia katika kilimo na kuondokana na umaskini na kujipatia ajira endelevu.

Linda Byaba aliendelea kusema lengo la kuendesha semina za kilimo ambazo sasa kupitia tawi letu la Iringa lililo maalumu kwa ajili ya mafunzo ya kilimo, ni kuhakikisha jamii inaondokana na kilimo cha mazoea na kujipatia maendeleo kwa kufikia kilimo cha biashara.